UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI KATIKA NYUGA ZA KIINSIA: HATARI ILIYOPO INAKABILIWA?
Abstract
Makala hii inakusudia kubainisha hatari inayozikabili nyuga za kiinsia. Hatari hiyo sio nyingine bali ni nyuga za kiinsia kupoteza umuhimu wake. Miongoni mwa ithibati ya kuwapo kwa hatari hii ni pamoja na idara mbalimbali za nyuga za kiinsia katika vyuo vikuu mbalimbali kufungwa. Aidha, katika nchi zinazoendelea, idadi ya udahili kwa wanafunzi wa nyuga za kiinsia imeshuka sana. Hii ni kutokana na serikali za nchi husika kupunguza au kuondosha kabisa ufadhili kwa wanafunzi hao. Makala imeonesha sababu za nyuga za kiinsia kuonekana kupoteza umuhimu wake kuwa ni pamoja na maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi yaliyosababisha thamani za nyuga kupimwa zaidi kwa faida za kiuchumi. Aidha, makala imeonesha namna ambavyo utetezi unaotolewa na wadau wa nyuga za kiinsia ambavyo umeonekana kutegemea zaidi huruma kuliko kudhihirisha namna ambavyo nyuga za kiinsia bado zina nafasi ya kufanikisha faida za kiuchumi. Hivyo basi, makala imeweka wazi sifa za wafanyakazi, maarifa yatakiwayo, na stadi zinazohitajika katika zama hizi za kidijiti. Hii imefanyika ili kutoa fursa kwa walimu, wataalamu, na wadau wengine wa nyunga za kiinsia, hususani katika vyuo vikuu, wapate nafasi ya kujifanyia tathimini iwapo kweli michakato yao ya ufundishaji na ujifunzaji inakabiliana na hatari hii iliyopo. Mwisho, makala inamalizia kwa kutoa mapendekezo ya nini kinapaswa kufanyika.