JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala
Jarida la Mnyampala (JM) ni jarida la kitaaluma lililopo chini ya idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha St John’s cha Tanzania. JM limesajiliwa na Maktaba Kuu ya Taifa mwaka 2019 na kupewa namba ya usajili ISSN 2683-6440 (nakala ngumu [print]) na e-ISSN 2683-6432 (nakala tepe ya mtandaoni [online]). Jarida limejikita katika uchapishaji wa makala za Fasihi, Isimu na Utamaduni wa Kiswahili. Hivyo basi, waandishi, watafiti na wapenzi wa Kiswahili wanakaribishwa kuchapisha makala katika jarida hili. Makala zote zitumwe kwa mhariri mkuu kupitia baruapepe jaridalamnyampala@sjut.ac.tz.
en-US JARIDA LA MNYAMPALA 2683-6440 UDHIHIRIKAJI WA MAMLAKA NA MAHUSIANO YALIYO NA UBISHI KUPITIA DHAMIRA NA NAMNA KATIKA USEMI https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/18
Makala inahusu dhamira na namna katika usemi na udhihirikaji wa mamlaka na mahusiano yanayowezeshwa kutokana na matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kanisa Katoliki kwenye nyumba za watawa za malezi. Kanisa Katoliki ni mojawapo ya asasi zenye desturi, sheria, itikadi, imani na kanuni zinazoliongoza. Uongozi wake hutekelezwa kutegemea ngazi zilizoko. Mojawapo ya viungo muhimu vya kanisa ni jamii ya watawa wenye viongozi katika mashirika kama Mama Mkuu, Makamu wa Mama Mkuu, Wasaidizi wa Mama Mkuu (washauri), viongozi wa maeneo na walezi. Aidha, kuna watawa walioweka nadhiri za daima, nadhiri za muda na walelewa. Watawa hutumia lugha ya Kiswahili katika mitagusano inayozalisha mahusiano kati yao. Kila lugha hudhihirisha itikadi na mamlaka na hutegemea nafasi ya mshirika katika asasi fulani kama nafasi ya kiongozi, daktari na washirika kudhihirisha lugha ya mamlaka waliyonayo (Fairclough, 1992). Ngazi za kiutawala kwa watawa zinadhihirisha mamlaka yaliyopo ya kitawa kupitia matumizi ya lugha ya Kiswahili katika usemi. Kutokana na hoja hii kulidhihirika ubishi katika mahusiano ya kimamlaka wakati wa mawasiliano baina ya walezi na walelewa katika usemi kupitia matumizi ya lugha ya Kiswahili (Wodak, 2001). Data zilikusanywa nyanjani katika nyumba za kitawa katika Jimbo Kuu la Mombasa katika Shirika la Masista wa Mt. Yosefu ambapo lugha ya Kiswahili hutumika kwa mapana. Matini hizi ziliangaliwa katika kiwango cha kishazi na sentensi kupitia dhamira na namna kwa mtazamo wa Sarufi Amilifu Msonge. Nadharia hii inajihusisha na wazo la uamilifu wa lugha. Je, kuna uwezekano wa ubishi wakati wa mawasiliano kati ya walezi na walelewa kwenye nyumba za watawa za malezi? Je, mamlaka na mahusiano hudhihirika vipi katika matumizi ya lugha yaliyo rasmi na yasiyo rasmi katika nyumba za watawa za malezi? Maswali haya ndiyo yalijibiwa katika makala.
Teresia W. Waweru John Habwe Iribe Mwangi Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 1 16 MICHAKATO YA KIFONOLOJIA INAYOATHIRI IRABU KATIKA MUUNDO WA VIVUMISHI VYA LUGHA ZA MNYAMBULIKO: MIFANO KUTOKA KIIMENTI https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/19
Kivumishi ni kipashio muhimu katika lugha kinachotumika pamoja na maneno mengine kufanikisha mawasiliano. Utafiti wa kifonolojia kuhusu kategoria mbalimbali za maneno ya lahaja za lugha ya Kimeru umewahi kufanywa. Kwa mfano, Wa Mberia (1981; 1993; 2002; 2015), Gacunku (2005) na Maore (2013) ni miongoni mwa wataalamu waliochanganua masuala ya kifonolojia katika lahaja mbalimbali za Kimeru. Hata hivyo, hatukupata utafiti uliochunguza muundo wa kivumishi cha lahaja ya Kiimenti ukiangazia michakato ya kifonolojia inayokumba kategoria hii ya maneno. Kwa hivyo, makala hii itanachunguza michakato mahususi ya kifonolojia inayokumba irabu pekee katika muundo wa kivumishi cha Kiimenti. Hii ni kwa sababu kivumishi cha Kiimenti hupitia mabadiliko mengi ya sauti kutoka muundo wake wa ndani hadi muundo wa nje. Aidha, makala hii inafafanua sheria zinazodhibiti mabadiliko hayo. Nadharia ya Fonolojia Zalishi Asilia (FZA) ya Hooper (1976) imetumika kuchanganua data katika makala hii. Data iliyochanganuliwa ilipatikana maktabani na uwandani. Maktabani, kazi mbalimbali zilizoangazia vivumishi vya Kiimenti zilichambuliwa. Utafiti wa uwandani ulifanyika katika wadi ya Abothuguchi Magharibi kwenye Kaunti ya Meru ambapo miktadha ya mikutano ya masoko, shule na makanisa iliteuliwa kimakusudi ili kukusanya data kuhusu vivumishi mbalimbali kutoka kwa wazungumzaji wazawa wa lahaja ya Kiimenti. Utafiti ulibainisha kuwa kuna michakato mingi ya kifonolojia inayopatikana katika vivumishi vya Kiimenti. Michakato hiyo huathiri irabu na konsonanti katika muundo wa vivumishi vya lahaja husika. makala hii itakuza na kuendeleza usomi wa vivumishi katika lugha mbalimbali za Kiafrika. Uelewa wa michakato ya kifonolojia inayoathiri irabu utasaidia kueleza kikamilifu muundo wa vivumishi vya Kiimenti na kuchochea utafiti zaidi kuhusu muundo wa vivumishi katika lugha za Kiafrika.
Kenneth Kinyua Thuranira James Ontieri Nancy Ayodi Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 17 40 UAINISHAJI WA MOFIMU KATIKA SENTENSI ZA KISWAHILI-KIINGEREZA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/20
Makala hii inalenga kuainisha mofimu katika sentensi zinazotokana na uhamishaji msimbo unaohusu lugha za Kiswahili na Kiingereza. Utafiti huu unaongozwa na Modeli  ya Kiunzi cha Lugha Msingi ya Myers-Scotton (1993) na modeli ya M-4 ya Myers- Scotton & Jake (2000). Kando na kuainisha mofimu katika sentensi za Kiswahili- Kiingereza, kazi hii pia inachunguza majukumu yanayotekelezwa na lugha za Kiswahili  na Kiingereza katika sentensi moja. Data ya utafiti huu imetokana na mazungumzo ya kawaida kutoka katika vipindi viwili vinavyoigizwa kwenye runinga ya NTV- Kenya ambavyo ni “The Wicked Edition” na “The Real Househelps of Kawangware.” Matokeo  ya uchunguzi huu yanadhihirisha kwamba mofimu katika sentensi za Kiswahili- Kiingereza zinaweza kuainishwa katika matapo manne makuu, yaani: mofimu za  kidhana, mofimu za kimfumo za mapema, mofimu mfumo za kidaraja na mofimu mfumo za nje. Kila aina ya mofimu hutekeleza jukumu mahususi. Hali kadhalika, lugha ya Kiswahili na ya Kiingereza huwa na uamilifu tofauti hivi kwamba lugha ya Kiswahili huitawala lugha ya Kiingereza kwa kuiwekea muundo wa kimofosintaksia ambamo mofimu za Kiingereza huchopekwa.
Shadrack Kirimi Nyagah Iribe Mwangi Basilio Gichobi Mungania Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 41 53 UCHANGANUZI WA MAKOSA YA MSAMIATI WA KISWAHILI KATIKA MATINI ANDISHI ZA HABARI: MFANO WA BBC SWAHILI NA DW KISWAHILI https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/21
Makala hii imechunguza makosa ya msamiati yanayofanyika katika vyombo vya habari vya BBC Swahili na DW Kiswahili. Istilahi msamiati, katika makala hii, inatumika kwa maana ya maneno yote yanayotumika katika lugha (TATAKI, 2013:384 na BAKITA, 2015:701). Malengo ya makala ilikuwa ni kuchanganua makosa ya msamiati, kubainisha sababu za makosa ya msamiati na athari za makosa hayo katika lugha. Ili kutimiza madhumuni ya Makala hii, kiunzi cha uchanganuzi wa habari kiisimu (van Dijk, 1988) kilizingatiwa. Sampuli ya utafiti huu ilihusisha matini ishirini za habari zilizosomwa kutoka kwenye tovuti za vyombo vya habari vilivyochunguzwa. Matokeo ya uchunguzi wa makala inaonesha kuwa vyombo vya habari vya BBC na DW (Idhaa za Kiswahili) hufanya makosa yanayohusu msamiati wa Kiswahili katika kuripoti habari kwa maandishi. Makosa hayo ni uunganishaji na utenganishaji wa maneno, uchopekaji na udondoshaji wa vipashio vinavyounda maneno, matumizi ya neno lisilofaa na utohozi wa maneno. Vilevile, makala ilibaini kwamba makosa hayo yalisababishwa na umilisi hafifu wa msamiati wa Kiswahili; athari ya lugha ya mazungumzo na lugha za kigeni. Mwisho, makala ilibaini kuwa makosa hayo yana athari kwa watumiaji wa Kiswahili na kupendekeza namna ya kuyaepuka.
Alcheraus R. Mushumbwa Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 54 71 LUGHA MKAKATI KATIKA MAWASILIANO YA CHOKORAA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/22
Makala hii inachunguza matumizi ya lugha mkakati katika mawasiliano ya chokoraa. Chokoraa huishi mitaani na hupitia changamoto mbalimbali zikiwamo unyanyapaa na ukosefu wa chakula. Kwa hali hii basi, chokoraa hufanya kazi kama vile kuwabebea wafanyabiashara wadogo bidhaa za kuuza na kuosha magari. Vile vile, chokoraa, wakati mwingine, huomba msaada kutoka kwa wanakundi-nje. Hali hizi mbalimbali ndizo huwafanya chokoraa kutumia lugha mkakati na kwa mitindo mbalimbali ili kutimiza nia zao za wakati husika. Data iliyokusanywa kuhusiana na mada hii inaonesha kuwa chokoraa hutumia lugha kutegemea muktadha wa mawasiliano. Tumebaini kuwa chokoraa hutumia lugha mkakati kwa kutumia mbinu kama vile kuchanganya ndimi, uradidi, matumizi ya majina yanayorejelea Mungu na vile vile matumizi ya lugha ya matusi kwa nia ya kupambana na unyanyapaa kutoka kwa wanakundi-nje. Kwa kufuata mkabala wa isimujamii, makala hii inaonesha kuwa chokoraa hutumia lugha mkakati ili kukidhi mahitaji yao ya wakati husika. Makala hii ni ya uchambuzi ubora na hivyo basi yalitumia data ambayo ilituwezesha kushughulikia mada hii. Data ambayo imetumiwa katika makala hii ilikusanywa na Ruth Binyanya baina ya Januari-Agosti, 2020 mtaani Mathare, jijini Nairobi kwa ajili ya tasnifu yake ya uzamivu ambapo alishughulikia matumizi ya lugha mkakati katika kutimiza nia mbalimbali za wanafamilia wa mitaani.
Ruth M. Binyanya Ayub Mukhwana Samuel M. Obuchi Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 72 87 UCHIPUZI WA KILEKSIKA KATIKA MASHAIRI YA SHAABAN ROBERT https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/23
Shaaban Robert ni miongoni mwa waandishi wenye hadhi ya juu katika fasihi ya Kiswahili kutokana na ukubwa na upevu wa mchango wake katika fasihi hiyo. Kuna tahakiki nyingi zikiwemo vitabu, tasnifu na makala ambazo zimeandikwa juu ya tungo zake. Hata hivyo, hatuwezi kusema kwamba uchunguzi juu ya kazi za kigogo huyo umetosha. Bado wahakiki wana kazi kubwa mbele yao. Shaaban Robert aliasisi na kuendeleza tanzu kama vile riwaya, wasifu, tawasifu na insha. Lakini ni katika ushairi ambapo alitoa mchango mkubwa zaidi. Tahakiki nyingi juu ya mashairi yake zinashughulikia maudhui zaidi kuliko fani. Mathalan: A. G. Gibbe (1980), E. K. Kezilahabi (1976) na F. E. M. K. Senkoro (1988). Hatusemi kwamba kuna ubaya wowote wa tahakiki kuelemea kwenye maudhui. Hata hivyo, kuna mengi sana katika fani ya mashairi ya Shaaban Robert ambayo yanastahili kushughulikiwa. Hivyo, mchango wa makala hii katika kuziba pengo hilo ni kuchunguza kipengele kimoja tu katika mtindo wa mashairi ya Shaaban Robert, yaani msamiati, na haswa jinsi mshairi anavyoepukana na ukawaida kutokana na ustadi wake wa kutumia lugha teule. Tunaitathmini leksisi hiyo kwa kuchunguza sababu za uteuzi na umuhimu wake wa kimaana. Kwa ujumla, mwelekeo wa makala ni wa elimumitindo.
Mwenda Mbatiah Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 88 103 SUALA LA UPOLE KATIKA FASIHI ANDISHI: UCHANGANUZI KATIKA RIWAYA YA PENDO LA KARAHA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/24
Makala hii inajadili suala la upole linavyojitokeza katika riwaya ya Pendo la karaha iliyoandikwa na John Habwe (2014). Misingi ya riwaya hii imejielekeza katika ukiukaji wa ukawaida ulioko katika jamii. Vijana wanatamani nafasi za kazi ughaibuni. Wanapofika huko, wanakumbana na changamoto nyingi na matarajio yao hayafikiwi. Kudra, bintiye Riziki na mhusika mkuu, anakata tamaa kutokana na kauli anazopokezwa na wanaomzunguka; naye Kassim anakata tamaa kutokana na vitendo anavyotendewa na mamaye, Rehema. Nadharia inayoongoza mjadala huu ni nadharia ya upole iliyoasisiwa na Brown & Levinson (1987). Makala inabainisha kauli zenye upole zinazotamkwa na wahusika mbalimbali, kuchunguza mikakati ya upole inayoteuliwa na wahusika katika mawasiliano yao na kutambua matendo yanayochangia kuwapo kwa upole katika mawasiliano baina ya wahusika. Kutokana na data zilizokusanywa, inaweza kuhitimishwa kuwa upole si suala la kiakademia tu, bali linaweza kuwa na umuhimu katika safu ya udiplomasia na katika masuala ya amani na maridhiano miongoni mwa wanajamii katika mataifa yetu na hata kimataifa.
Agnes Mueni Muteti Evans M. Mbuthia Mary Ndung’u Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 104 121 KISWAHILI KATIKA MATAMASHA YA MAIGIZO YA SHULE NA VYUO NCHINI KENYA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/25
Matamasha ya shule na vyuo nchini Kenya huandaliwa kila mwaka kati ya Januari na Aprili. Matamasha haya hushirikisha kila shule na vyuo vya serikali pamoja na vya binafsi. Matamasha haya yalianzishwa mwaka wa 1959. Huu ulikuwa wakati wa ukoloni na kwa sababu hii, maigizo yalitawaliwa na sifa za matamasha na maigizo ya Uingereza yaliyoshirikisha taasisi za elimu ya juu. Matamasha ya mwanzo mwanzo nchini Kenya yalishirikisha taasisi za Wazungu na Wahindi pekee. Baada ya uhuru, matamasha haya yalianza kushirikisha shule na taasisi za Kiafrika. Ingawaje lugha za Kiafrika zimekubaliwa kushirikishwa katika tungo za kuwasilishwa katika matamasha haya, mawasilisho mengi huwa katika lugha ya Kiingereza. Hali hii imewacha Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika zikikosa kushirikishwa kikamilifu. Makala basi inajadili nafasi ya Kiswahili katika ujenzi wa taifa kupitia kwa matamasha haya.
Mosol Kandagor Toboso Mahero Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 122 133 RIWAYA YA KISWAHILI: JICHO FICHUZI NA ANGAZI LA VIVUTIO VYA UTALII ZANZIBAR https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/26
Lugha ya Kiswahili na fasihi yake zinajengana. Kukua kwa lugha ya Kiswahili kunaimarisha ukuaji wa fasihi ya Kiswahili. Kwa upande mwingine, kukua kwa fasihi ya Kiswahili kunaimarisha pia maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Kwa pamoja, maendeleo ya lugha ya Kiswahili na fasihi yake yanachangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa sekta ya utalii ambayo inachangia kukua kwa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Fasihi ya Kiswahili, hasa riwaya, ina mchango mkubwa katika kuvifichua, kuvionesha, kuvitangaza na kuvieleza vivutio vya utalii katika visiwa vya Zanzibar. Hatimaye, watalii wa ndani na nje ya nchi, hutembelea na kuchangia pato la taifa na la watu binafsi. Makala inaangalia namna baadhi ya riwaya za Kiswahili za Zanzibar zilivyoibua na kuvitangaza vivutio vya utalii visiwani Zanzibar na hatimaye kuimarika kwa uchumi wake. Data za makala imekusanywa kwa njia ya udurusu wa matini za riwaya teule nne: Kiu (1972), Asali chungu (1977), Vuta n’kuvute (1999), na Kosa la bwana Msa (1984). Nadharia ya uhalisia imetumiwa kuongoza uchambuzi wa data katika makala hii. Makala inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika fasihi ya Kiswahili na uimarishaji wa sekta ya utalii Afrika ya Mashariki hasa katika kipindi hiki cha hamasa ya uchumi wa buluu Zanzibar.
Masoud Nassor Mohammed Geofrey Kitula King’ei Copyright (c) 2024 2023-05-31 2023-05-31 3 134 149