JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala
Jarida la Mnyampala (JM) ni jarida la kitaaluma lililopo chini ya idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha St John’s cha Tanzania. JM limesajiliwa na Maktaba Kuu ya Taifa mwaka 2019 na kupewa namba ya usajili ISSN 2683-6440 (nakala ngumu [print]) na e-ISSN 2683-6432 (nakala tepe ya mtandaoni [online]). Jarida limejikita katika uchapishaji wa makala za Fasihi, Isimu na Utamaduni wa Kiswahili. Hivyo basi, waandishi, watafiti na wapenzi wa Kiswahili wanakaribishwa kuchapisha makala katika jarida hili. Makala zote zitumwe kwa mhariri mkuu kupitia baruapepe jaridalamnyampala@sjut.ac.tz.
en-US jaridalamnyampala@sjut.ac.tz (Dkt. Shadidu A. Ndossa) jkungura@sjut.ac.tz (Johnkenedy kungura) Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 OJS 3.3.0.8 http://blogs.law.harvard.edu/tech/rss 60 NAFASI YA JAZANDA KATIKA UWASILISHAJI WA MAUDHUI YA MAPENZI NA MAUMIVU YA KIHISIA: MIFANO KUTOKA WIMBO WA KIZA KINENE https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/45
Makala hii inajadili matumizi ya jazanda katika wimbo wa Kiza Kinene wa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania, Nandy, kwa kushirikiana na kundi la muziki la Sauti Sol kutoka Kenya. Kwa kutumia Nadharia ya Uhakiki wa Fasihi Jamii, makala inatathmini jinsi jazanda zinavyotumika kama mbinu ya kisanaa katika kuakisi mazingira halisi ya kijamii, kihisia na kiutamaduni ya wasanii na jamii zao. Aidha, makala inaonesha kuwa jazanda zilizopo katika wimbo huu zinahusiana na viungo vya mwili, mazingira ya asili, familia, biashara na imani za jadi, zikielezea kwa kina hisia za maumivu, upweke, usaliti na matarajio yaliyofifia katika mapenzi. Makala inahitimisha kuwa jazanda si mapambo ya lugha pekee bali ni nyenzo muhimu ya mawasiliano yenye mguso wa kijamii, kiitikadi na kihisia, inayomwezesha msanii kuwasilisha ujumbe mzito kwa namna ya ubunifu na isiyo ya moja kwa moja.
Shadidu A. Ndossa Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/45 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 CHANGAMOTO ZA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA KISWAHILI KAMA LUGHA YA PILI KATIKA SHULE ZA UPILI NCHINI RWANDA: MFANO WA SHULE TEULE WILAYANI MUSANZE https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/46
Makala hii inalenga kujadili changamoto zinazowakumba walimu na wanafunzi katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya pili nchini Rwanda, mfano wa shule teule za upili wilayani Musanze. Aidha, makala hii iliongozwa na Nadharia ya Viwezeshi katika ufundishaji wa lugha iliyoasisiwa na Gibson katika mwaka wa 1977. Vilevile, wakati wa ukusanyaji wa data, mtafiti alitumia ushuhudiaji, usaili na uchanganuzi matini kama mbinu za kukusanya data. Walengwa walikuwa walimu na wanafunzi kutoka shule teule za G S Muhoza I na Ecole de Sciences de Musanze, wilayani Musanze. Data za watafitiwa zilifanyiwa uchanganuzi na matokeo yalibainisha kuwa walimu na wanafunzi wote hukumbwa na changamoto tofauti wakati wa ufundishaji wa Kiswahili. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa nyenzo za kufundishia na kujifunzia, ujuzi finyu wa lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi, ukosefu wa mafunzo kwa walimu na mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu lugha ya Kiswahili. Makala, inapendekeza kuboresha ufundishaji wa Kiswahili nchini kwa kuchapisha vitabu vingi zaidi, kutoa mafunzo kwa walimu wa Kiswahili na kuongeza idadi ya vipindi vya Kiswahili. Pia, kuhakikisha kuwa Kiswahili kinatahiniwa katika mitihani ya taifa kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha tatu.
Faustin Ndikubwimana Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/46 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 UKALIMANI KATIKA MAHUBIRI KANISANI: UPOTOSHI AU UPANUZI WA MAANA? https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/47
Makala hii inachunguza mchango wa dini katika lugha ya Kiswahili. Mchango wa dini katika maisha ya binadamu huwamba nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Dini imekuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya Kiswahili, hasa kupitia tafsiri na ukalimani, tangu enzi za ukoloni na ujio wa Wamishonari. Ukalimani wa kijamii, hususan katika mahubiri, huathiri Kiswahili ama kwa kukikuza au kukidumaza kimsamiati na kisarufi. Wakati mwingine, mkalimani hukosa muda wa kupitia na kusahihisha tafsiri yake, na kuleta tafsiri isiyokusudiwa. Mbali na umilisi wa lugha chanzi na pokezi, tafsiri humhitaji mfasiri kusomea tafsiri. Kwa hiyo, ukosefu wa muda hauwezi kuwa idhini kwa mkalimani kutepetea kwa sababu ujumbe unaokusudiwa na mzungumzaji ndio huwa muhimu zaidi. Mahubiri yanapokalimaniwa, lugha hutumiwa kiholela, na wakati mwingine inabadilisha maana inayokusudiwa. Lengo la makala hii ni kubainisha matumizi maalum ya lugha katika tafsiri za kidini, kutathmini iwapo matumizi hayo yanapanua au kupotosha Kiswahili kimsamiati na kimaana, na kutoa mapendekezo yatakayoboresha ukalimani wa mahubiri ya kidini ili kuchangia ukuaji wa lugha ya Kiswahili. Uchunguzi umejikita katika makanisa ya kiroho mjini Kakamega ambako mahubiri yalisikilizwa na kurekodiwa katika miktadha yake ya asili. Katika utafiti huu, data zilikusanywa kwa njia ya usikilizaji na kurekodi mahubiri katika miktadha yake ya asili. Kisha, muundo wa kimaelezo ulitumika kuchanganua data ili kutoa uelewa wa athari za ukalimani katika maendeleo ya Kiswahili.
Moses Wamalwa Wasike, Mark Mosol Kandagor, Magdaline Nakhumicha Wafula Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/47 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 UFUTUHI: SILAHA YA JADI ILIYOTUMIWA NA SHAABAN ROBERT KUPAMBANA NA UKOLONI https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/48
Makala hii inabainisha namna mbinu ya ufutuhi ilivyotumika kama silaha ya kijadi ya kupambana na ukoloni. Utafiti uliozalisha makala hii ulitumia Nadharia ya Uhemenitiki. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu mbili, usaili na uchambuzi wa matini, kisha kuchanganuliwa kwa kutumia mbinu ya usimbishaji wa maudhui. Inabainishwa katika makala hii kuwa riwaya ya Kusadikika ni shambulizi kali lililoelekezwa kwa wakoloni, ambapo Shaaban Robert anabeua na kuing’ong’a mifumo ya kikoloni. Aidha, anaizindua jamii kuhusu umuhimu wa kujipapatua kutoka kwenye mikatale ya kikoloni. Kutokana na miktadha mbalimbali ya kikoloni iliyokuwa inamzunguka, aliweza kupenyeza shambulizi kwa maadui zake kwa kutumia aina nne za ufutuhi: ufutuhi wa majazi, ufutuhi wa balagha, ufutuhi wa unyume, na ufutuhi wa utanakuzi. Makala inahitimisha kwa kuwahamasisha waandishi ambao ni miongoni mwa makundi yanayotegemewa zaidi na jamii katika kuiongoza, kuikosoa, na kuiokomboa, kuendelea kuvaa ujasiri wa kufanya kazi yao kwa kutumia mbinu anuwai.
Athumani S. Ponera Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/48 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 DAVID MASSAMBA: MWANAISIMU MWENYE HAZINA FICHE KATIKA FASIHI YA KISWAHILI https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/49
Watu wengi wanamfahamu Hayati Prof. David Massamba kama mwanazuoni aliyemakinikia uga wa isimu kwa kiwango kikubwa huku baadhi ya vitabu vyake vikiwa maarufu katika ulimwengu wa Kiswahili. Hata hivyo, lipo jambo ambalo watu wengi hawalijui kwa mwanazuoni huyu; nalo ni suala la kujikita kwake katika kuandika kazi za kifasihi, hususani uga wa ushairi. Kwa hiyo, lengo la makala hii ni kubainisha na kuelezea hazina iliyojificha ya Massamba ili watu wapate kuijua na kuitumia kama ambavyo wanatumia maarifa yake ya isimu. Makala hii ni matokeo ya utafiti wa maktabani ambapo waandishi wametalii kazi mbalimbali za Massamba katika isimu na fasihi. Data zimechanganuliwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli chini ya Nadharia ya Uwasifu. Imebainika kwamba Massamba ana hazina fiche katika fasihi hususani katika ushairi wa Kiswahili ambapo ameandika Diwani ya Massamba na makala ya kinadharia inayohusiana na utunzi wa ushairi wa Kiswahili. Makala hii imejaribu kutoa muhtasari wa kazi hizo ili kuwahamasisha watu kusoma na kujipatia maarifa yaliyomo katika kazi hizo za kifasihi za Massamba.
Issaya Lupogo, Hassan R. Hassan Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/49 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 TATHIMINI YA SABABU ZA KUFANYIKA KWA MAKOSA YA KIMATAMSHI NA KIOTHOGRAFIA KATIKA KISWAHILI: MFANO WA SHULE TEULE ZA SEKONDARI WILAYANI NYARUGENGE NCHINI RWANDA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/50
Makala imechunguza sababu za kufanyika kwa makosa ya kimatamshi na kiothografia katika lugha Kiswahili. Tafiti nyingi zilizofanyika zilijikita zaidi katika uchanganuzi wa makosa ya kimatamshi na kiothografia yanayofanyika katika Kiswahili bila kutoa sababu zinazosababisha makosa hayo. Kutokana na hayo, utafiti wetu ulitathmini vyanzo vya kufanyika kwa makosa ya kimatamshi na kiothografia miongoni mwa wanafunzi wanaosoma Kiswahili kama lugha yao ya pili. Makala iliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa iliyoasisiwa na Corder mnamo mwaka 1967. Sampuli ya watafitiwa ilihusisha walimu 6 wa Kiswahili na wanafunzi 15 kutoka shule teule tano tofauti. Shule hizi ziliteuliwa kwa kuwa zinakaa katika eneo lenye Waislamu wengi ambao ni wazungumzaji wakubwa wa Kiswahili. Shule hizo zilikuwa Gs. Camp Kigali, Gs. Cyahafi, Shule ya Kiufundi ya Leading, Lycée Notre Dame de Citeaux na Epa St Michel. Data zilikusanywa kwa kutumia mahojiano, ushuhudiaji na udurusu wa nyaraka. Matokeo ya utafiti yalibainisha kuwa makosa ya kimatamshi na kiothografia katika Kiswahili yanatokana na ujuzi finyu wa lugha lengwa, kutojua kanuni za kisarufi, ukiukaji wa kanuni za kisarufi, uhamishaji wa vipengele vya lugha ya kwanza kwa lugha ya pili, wingilugha katika ujifunzaji wa Kiswahili pamoja na mtazamo hasi dhidi ya lugha ya Kiswahili.
Pascal Sebazungu Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/50 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 MCHANGO WA TEHAMA KATIKA UFUNDISHAJI WA FASIHI ANDISHI YA KISWAHILLI KATIKA SHULE ZA SEKONDARI TEULE WILAYANI NYAGATARE NCHINI RWANDA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/51
Makala hii inaangazia mchango wa TEHAMA katika ufundishaji wa fasihi andishi katika shule za sekondari wilayani Nyagatare, Rwanda. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Uunganisho, ukitumia mbinu za usaili, ushuhudiaji, na uchanganuzi wa matini kukusanya data. Sampuli ilijumuisha wanafunzi 103, walimu wa Kiswahili 5 na wakuu wa masomo 5 walioteuliwa kwa usampulishaji lengwa. Data zilizokusanywa kwa usaili na uchanganuzi wa matini, zilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa madondoo na maelezo. Matokeo yameonesha kwamba TEHAMA huchangia pakubwa katika ufundishaji wa fasihi andishi. Inarahisisha upatikanaji wa nyenzo za kielimu kama vitabu vya kielektroni na video, huwezesha wanafunzi kuwasiliana na wenzao kimataifa, na kuwasaidia kujifunza stadi mpya. Aidha, TEHAMA huwapa wanafunzi motisha na kuifanya fasihi kuwa ya kuvutia zaidi. Hata hivyo, changamoto zilibainika, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa zana za kufundishia na mbinu duni za walimu. Ili kukabiliana na changamoto hizi, utafiti umependekeza maandalizi ya warsha za TEHAMA na kuboresha miundombinu shuleni. Matokeo haya yanaonesha umuhimu wa TEHAMA katika kuimarisha ufundishaji wa fasihi andishi na kutatua changamoto zilizopo.
Tulinumukiza Frodouard, Wallace K. Mlaga Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/51 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000 MAKOSA YA KISEMANTIKI YANAYOFANYWA NA WANAFUNZI WA KISWAHILI: MIFANO KUTOKA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI TEULE NCHINI RWANDA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/52
Makosa yanayojitokeza katika ujifunzaji wa lugha ya pili ni yale ya kifonolojia, kimofosintaksia, kisemantiki, na kiotografia (Corder, 1980; na Niyomugabo, 2016). Naye, Wray (2000) anaeleza kuwa katika uchunguzi wa makosa ya kilugha, baadhi ya tafiti zilizofanywa hazikushughulikia semantiki. Hivyo, makala hii inachanganua makosa ya kisemantiki yanayofanywa na wanafunzi wa Kiswahili katika shule za sekondari nchini Rwanda. Malengo yake ni kubainisha aina za makosa ya kisemantiki yanayofanywa na kiwango cha makosa hayo yanavyoathiri umahiri wa wanafunzi wa Kiswahili. Mbinu zilizotumiwa kukusanya data ni mahojiano, ushuhudiaji na uchambuzi matini. Data zilizokusanywa zilichambuliwa na kutolewa maelezo kwa kutumia misingi ya Nadharia ya Uchanganuzi Makosa iliyoasisiwa na Corder (1967). Matokeo ya data zilizochambuliwa yalionyesha kuwa makosa ya kisemantiki yanayowakabili wanafunzi katika ujifunzaji wa Kiswahili yanasababisha changamoto za kisemantiki kwa wanafunzi Wanyarwanda katika ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Makosa yaliyobainishwa ni tafsiri kutoka lugha ya kwanza, makosa ya kimuundo, makosa ya kisemantiki leksia, kutumia sauti isiyofaa katika neno, makosa ya kutumia lugha ya kishairi na makosa ya kunukuu. Pia, makala imeonyesha kiwango cha wanafunzi cha kuathiriwa na makosa hayo. Kutokana na matokeo haya, imependekezwa kwamba ngazi mbalimbali zinazohusiana na ufundishaji na ujifunzaji ili kushirikiana kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Vivens Niyotugira, Sylvain Ntawiyanga Copyright (c) 2024 JARIDA LA MNYAMPALA https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/52 Mon, 30 Dec 2024 00:00:00 +0000