HADHIRA YA USHAIRI HURU WA KISWAHILI NI IPI?
Abstract
Makala hii inaangazia mustakabali wa hadhira katika upokezi wa ushairi huru wa Kiswahili. Mwanzoni mwa miaka 1970, ushairi huu ulijitokeza kwa kasi na ulituhumiwa kwa kutozingatia arudhi za kimapokeo. Watunzi wa awali wa ushairi huu walikuwa wataalamu wa lugha na wahakiki wa fasihi; waliotoa maelezo muhimu kuhusu dhana na sifa za ushairi wa Kiswahili. Kabla ya miaka 1960, ushairi wa kimapokeo ulikuwa umesambaa na umezoewa katika jamii. Kujitokeza kwa ushairi huru kulisababisha watunzi na hadhira kugawanyika katika makundi: lile linalojinasibisha na arudhi, lile lisilojinasibisha na arudhi, na lile linalojinasibisha kwa kiasi na arudhi hizo. Katika miaka ya 1970, waliouendeleza zaidi ushairi huru walikuwa ‘vijana’ waliobahatika kupata elimu ya juu katika taaluma ya fasihi na walitarajia kuchangia katika ufafanuzi wa dhana na sifa za ushairi wa Kiswahili kwa ujumla. Swali linalofafanuliwa katika makala hii ni: kwa nini ushairi huru wa Kiswahili ni kivutio cha wataalamu wa lugha na wahakiki wa fasihi? Nadharia ya Semiotiki imetumika kufafanulia matini za lugha kama viishara na viashiria vinavyohitaji kufasiriwa. Data ya uchanganuzi ilitokana na upitiaji wa mashairi katika diwani teule za mashairi ya Kiswahili. Aidha, data nyingine ilitokana na usaili na hojaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wataalamu wa lugha na fasihi.