TATHMINI YA TAFSIRI YA JALADA LA KITABU: MIFANO KUTOKA TAFSIRI YA THE BLACK HERMIT (THIONG`O, 1968) NA KIFO KISIMANI (MBERIA, 2001)
Abstract
Lengo kuu la tafsiri ni kufanikisha mawasiliano kwa sababu hadhira lengwa haijui lugha wala utamaduni chanzi. Hivyo, mfasiri anapaswa kuwa mwaminifu kwa kulinda ukweli na ufasaha wa ujumbe wa matini chanzi katika matini lengwa. Ujumbe huo hubebwa na vipashio mbalimbali (maneno, virai, sentensi na aya) ambavyo mfasiri hana budi kuvizingatia. Aidha, mfasiri huzingatia vipengele vya lugha na masilugha vilivyomo katika jalada la tafsiri ili aweze kuandaa jalada la matini lengwa linaloendana na ujumbe wa jalada la matini chanzi. Hii ni kwa sababu jalada hubeba maana na ujumbe ulio kamili kwa kutumia lugha na masilugha. Hivyo basi, makala hii imetathmini tafsiri ya jalada la tafsiri ya tamthiliya ya The Black Hermit iliyoandikwa na Ngugi wa Thiong`o (1968), kisha ikatafsiriwa kama Mtawa Mweusi na Ngugi wa Thiong`o (1970) na tamthiliya ya Kifo Kisimani iliyoandikwa na Kithaka wa Mberia (2001) na ikatafsiriwa kama Death at the Well na Khalfan Kasu (2011). Tathmini imefanywa kwa kuchunguza kufanana na kutofautiana kwa tafsiri za majalada kati ya matini chanzi na matini lengwa. Makala hii imeongozwa na Nadharia ya Usawe wa Kidhima iliyoasisiwa na Nida (1964). Data imekusanywa kwa kutumia mbinu ya usomaji matini. Uchambuzi wa data hiyo umetumia mbinu linganishi na mkabala wa kitaamuli. Hatimaye, makala imebaini kuwa, licha ya vipengele kadhaa kufanana, bado kuna tofauti zinazojitokeza katika tafsiri hizo. Jambo hili linasababisha kutowiana kwa baadhi ya maudhui ya MC na ML. Hivyo, makala inapendekeza kwamba si kila jalada lazima litafsiriwe. Kutafsiriwa ama kutotafsiriwa kwa jalada la kitabu kunategemea muktadha wa tafsiri husika.