ATHARI ZA MFUMO WA VIHUSISHI VYA KINANDI KATIKA UAMILIAJI WA KISWAHILI KAMA L2 MIONGONI MWA WANAFUNZI WANAOSEMA KINANDI KAMA L1
Abstract
Uamiliaji wa L2 ni tukio lisiloepukika katika karne ya sasa yenye migusano mingi ya lugha inayosababishwa na mitagusano ya watu wanaosema lugha tofauti na kupitia ujifunzaji na ubwiaji wa lugha. Uamiliaji wa L2 ni zao la maendeleo ya binadamu, kijamii, kiuchumi na kisiasa. Maendeleo haya hulazimisha nchi na watu kujifunza lugha nyingine ili mahitaji fulani ya maendeleo yaweze kuafikiwa. Uamilijia huu unakuwa wa lazima ili watu wanaosema lugha tofauti waweze kuelewana na kubadilishana mawazo. Mwamiliaji wa L2 mara nyingi hukumbwa na changamoto ya kuathiriwa na mfumo wa kiisimu wa LI. Athari kutoka L1 ni za kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki, ambazo zinamwaathiri mwamiliaji wa L2. Makala hii imeshughulikia athari za kimofosintaksia za mfumo wa vihusishi vya Kinandi katika insha za Kiswahili za wanafunzi wanaosema Kinandi kama L1. Ni zao la utafiti uliofanywa katika shule tatu za msingi katika Kaunti ya Nandi nchini Kenya kwa minajili ya kuandaa tasnifu ya uzamili. Katika utafiti huo, shule hizi zilirejelewa kwa akronimu NSB. Utafiti huo ulibainisha changamoto nyingi za kiisimu-nafsia katika kiwango cha kimofosintaksia zinazomkumba mwanafunzi anayesema Kinandi kama L1 anapoamilia Kiswahili kama L2. Mojawapo ya vyanzo vya changamoto hizi ni athari za mfumo wa vihusishi vya Kinandi zinazojadiliwa katika makala hii.