MATUMIZI YA LUGHA YA VIJANA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA SEKONDARI TANZANIA
Abstract
Makala hii imejadili matumizi ya lugha ya vijana wa shule za sekondari nchini Tanzania, na mambo yanayosababisha matumizi hayo. Cheshire (1982) na Milroy (1978, 1987) wanaeleza kuwa utofauti wa lugha hutokana na mahusiano yaliyopo katika kundi linalohusika ambapo hutegemea mila, desturi, na kaida ambazo hufanana katika kundi hilo na kufanya kuwapo kwa matumizi tofauti ya lugha katika matamshi, msamiati na tungo. Makala hii imetumia data kutoka uwandani zinazohusu matumizi ya lugha ya vijana wa sekondari wilaya ya Morogoro. Nadharia ya Milroy (1980) inayohusu mitandao ya kijamii imetumika kuchambua data hizo. Makala hii imebaini kuwa vijana wa sekondari wana matamshi, msamiati na tungo wanazozitumia katika mazungumzo yao ambazo hutofautiana na zile za marika mengine. Hali hii husababishwa na haja ya kuwa na usiri au kuficha maana iliyokusudiwa, ucheshi na utani, kuonesha mshikamano na mazoea yaliyojengeka miongoni mwao.