MIKAKATI, CHANGAMOTO NA MUSTAKABALI WA UTUNGAJI WA KAMUSI ZA KIISTILAHI ZA KISWAHILI
Abstract
Maendeleo katika taaluma ya leksikografia yamepelekea kuwapo kwa idadi kubwa ya kamusi za istilahi za Kiswahili katika nyanja za taaluma mbalimbali. Hata hivyo, licha ya maendeleo hayo, hakuna kamusi kamilifu isiyo na upungufu wa aina fulani. Kwa kutumia mbinu za utafiti wa maktabani, makala hii imefafanua mikakati, changamoto na mustakabali wa utungaji wa kamusi za kiistilahi za Kiswahili. Lengo lake ni kubainisha mbinu zinazofaa zaidi katika utungaji kamusi za istilahi za Kiswahili zitakazokidhi mahitaji ya lugha hiyo katika kipindi hiki na siku za usoni. Hoja kuu ya makala hii ni kwamba kuegemea zaidi kwenye mbinu za tafsiri na zile za kileksikografia badala ya zile za kiteminografia katika utungaji wa kamusi za istilahi za Kiswahili kumetinga ufanisi katika sayansi na sanaa hiyo. Data iliyotumika ni mifano ya istilahi za kompyuta zilizoorodheshwa kama vidahizo katika Kamusi Sanifu ya Kompyuta (Kiputiputi, 2011). Imedhihirika kwamba ubora au upungufu wa kamusi ya kiistilahi hutegemea maumbo ya vidahizo vilivyomo, fasili zake, uzingatiaji wa mifumo na vikoa vya dhana na muundo wa vitomeo vyake. Kwa hivyo, kamusi za kiistilahi za siku za baadaye zitakuwa na mwelekeo wa kuwa mediatutiko, mkondoni na zenye uwezo kusasaishwa kuendana na maendeleo katika uwanja wa taaluma inayohusika.