MTANGAMANO KAMA KIUNGO CHA MSHIKAMANO KATIKA DISKOSI ZA KIWINGI-LUGHA
Abstract
Mshikamano ni elementi muhimu ya kiisimu inayochangia ufasili wa maana katika diskosi. Makala hii, hivyo basi, inafafanua jinsi mtangamano unavyohusika kama kiungo cha mshikamano katika diskosi za kiwingi-lugha. Nadharia Amilifu Zalishi ilitumiwa katika uchunguzi huu (Sawe, 2015). Nadharia hiyo inasisitiza kwamba uunganishaji, uradidi na mtangamano ni mikakati inayojenga mshikamano katika matini au diskosi huku ikipinga dai kwamba udondoshaji ni kijenzi cha mshikamano. Data ilikusanywa kutoka sampuli ya makanisa mawili na vyuo vikuu viwili nchini Kenya. Diskosi za kiwingi-lugha za wanafunzi waliozungumza Kiswahili, Kikipsigis na Kiingereza zilichunguzwa. Utafiti huu uligundua kwamba wanawingi-lugha hutumia mtangamano kama mojawapo ya mikakati ya kuendeleza mshikamano katika mazungumzo yao yenye ubadilishaji msimbo.