DHANA YA UHUSIKA KATIKA KAULI YA KUTENDEA
Abstract
Dhana ya uhusika ina utata katika machapisho wa Kiswahili. Hii ni kwa sababu wakati mwingine ikifasiliwa kuwa ni dhana ya kimuundo, na wakati mwingine, ni dhana ya kisemantiki. Makala hii inapendekeza kuichukulia dhana hiyo kuwa ni ya kimuundo na dhana ya ushiriki kuwa ni ya kisemantiki. Dhana hizo mbili zinaelezwa kwa kutumia mifano kutoka kauli ya kutendea. Unyambulishaji wa kutendea husababisha kitenzi kupata yambwa mpya. Yambwa mpya inaweza kutafsiriwa kwa namna mbalimbali kutokana na uhusiano wa yambwa hiyo na kitenzi. Kwa kutumia uhusiano mbalimbali wa yambwa na vitenzi, inaonesha kwamba uhusika wa ala waweza kuwa wa namna mbalimbali. Ushahidi unaotokana na uchambuzi wa sentensi za utendea na yambwa mbadala unadhihirisha kwamba tofauti za ushiriki zinatokana na maana ya mzizi wa kitenzi na hulka za nomino ninazohusika katika matukio.