SAUTI YA DHIKI: HAZINA YA KUHIFADHI, KUKABILI NA KUFUATILIA MAOVU YOTE KWA NJIA YA AMANI
Abstract
Kenya imepitia kipindi kisicho mfano cha kukiukwa kwa haki za binadamu. Hili limedhihirika kupitia migogoro na mizozo ya mara kwa mara ya kikabila. Ukiukwaji huu unajumuisha mauaji ya halaiki, mateso, uovu, pamoja na uhalifu wa aina mbalimbali. Kwa kuzingatia ukweli huu, wasanii, wakiwemo washairi, pia wanajitokeza kuchangia katika suala hili. Kwa kutumia diwani ya Sauti ya Dhiki (Abdalla, 1973), makala hii inatalii jinsi dhuluma na kususia huwasilishwa kishairi. Ushairi wa Kiswahili unajitokeza kama chombo cha kuangazia dhuluma mbalimbali za kijamii na za kisiasa na kama njia ya kuelezea hisia za kibinafsi kuhusu dhuluma. Ushairi unasomwa kama njia ya kuwawezesha watu kuasi na kupinga hali na mifumo inayowakandamiza, kuwasilishia yasiyowasilishika, na kutoa sauti mbadala ya kuelezea masuala yanayoisakama jamii.
Lugha na Sanaa ya Kusema “La! kwa Ukatili”
Historia ya Kenya imejaa visa vya mauaji ya kutisha ambayo baadhi yake yanasemekana kuwa yalifadhiliwa na vyombo vya usalama kwa kisingizio cha oparesheni ya usalama. Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Haki na Maridhiano, utawala wa serikali mbalimbali umechukuliwa kuwa mwendelezo wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu (TJRC, 2013). Ukiukaji huu umejitokeza kupitia vita3, mauaji4, mateso5, adhabu ya pamoja, kumnyima mtu mahitaji ya msingi, mauaji ya kisiasa,6 kutia mtu kizuizini, dhuluma pamoja na unyanyasaji wa wapinzani wa kisiasa na wanaharakati wa haki za binadamu. Orodha hii ndefu ya visa vya ukatili imevuta makini ya washairi ambao wana jukumu la kuwa sauti ya mnyonge. Uchunguzi wa tungo za fasihi ya Kiswahili unaonyesha matukio ambapo Waswahili walitumia sanaa zao kudai uhuru wao wa kisiasa na wa kiuchumi. Ushairi ulijitokeza kama njia ambayo kwayo msanii aliwapatia sauti ‘wanaoteswa’ (Dawes, 2007). Makala hii inafafanua jinsi suala hili la ukatili lilivyoangaziwa katika Sauti ya Dhiki. Diwani hii ilitungwa na Abdilatif Abdalla baada ya ukoloni nchini Kenya. Ingawa hii ni diwani ya mwandishi mmoja tu, ina data za kutosha
3 Mifano ni pamoja na vita vya Maumau na vya Mashifta.
4 Haya ni pamoja na mauaji ya Kedong, Ususiaji wa Giriama, Mauaji ya Kollowa, ya Lari, ya Hola, ya Turbi na ya Bubisa (2005), ya Murkutwa (2001), ya Loteteleit (1988), ya Bulla Karatasi (1980), ya Wagalla, (1984), ya Lotirir (1984) ya Malka Mari (1981), na ya Garissa (1980).
5 Hasa vyumba katika majengo ya Nyayo na Nyati vilivyotumiwa kuwatesa wapinzani.
6 Waliouawa ni pamoja na Pio Gama Pinto, Tom Mboya, J.M. Kariuki, Dr. Robert Ouko, Askofu Alexander Muge Crispine Odhiambo Mbai, na Padri John Kaiser.