MICHAKATO YA KIFONOLOJIA INAYOATHIRI IRABU KATIKA MUUNDO WA VIVUMISHI VYA LUGHA ZA MNYAMBULIKO: MIFANO KUTOKA KIIMENTI

Authors

  • Kenneth Kinyua Thuranira Chuo Kikuu cha Maasai Mara
  • James Ontieri Chuo Kikuu cha Rongo
  • Nancy Ayodi Chuo Kikuu cha Maasai Mara

Abstract

Kivumishi ni kipashio muhimu katika lugha kinachotumika pamoja na maneno mengine kufanikisha mawasiliano. Utafiti wa kifonolojia kuhusu kategoria mbalimbali za maneno ya lahaja za lugha ya Kimeru umewahi kufanywa. Kwa mfano, Wa Mberia (1981; 1993; 2002; 2015), Gacunku (2005) na Maore (2013) ni miongoni mwa wataalamu waliochanganua masuala ya kifonolojia katika lahaja mbalimbali za Kimeru. Hata hivyo, hatukupata utafiti uliochunguza muundo wa kivumishi cha lahaja ya Kiimenti ukiangazia michakato ya kifonolojia inayokumba kategoria hii ya maneno. Kwa hivyo, makala hii itanachunguza michakato mahususi ya kifonolojia inayokumba irabu pekee katika muundo wa kivumishi cha Kiimenti. Hii ni kwa sababu kivumishi cha Kiimenti hupitia mabadiliko mengi ya sauti kutoka muundo wake wa ndani hadi muundo wa nje. Aidha, makala hii inafafanua sheria zinazodhibiti mabadiliko hayo. Nadharia ya Fonolojia Zalishi Asilia (FZA) ya Hooper (1976) imetumika kuchanganua data katika makala hii. Data iliyochanganuliwa ilipatikana maktabani na uwandani. Maktabani, kazi mbalimbali zilizoangazia vivumishi vya Kiimenti zilichambuliwa. Utafiti wa uwandani ulifanyika katika wadi ya Abothuguchi Magharibi kwenye Kaunti ya Meru ambapo miktadha ya mikutano ya masoko, shule na makanisa iliteuliwa kimakusudi ili kukusanya data kuhusu vivumishi mbalimbali kutoka kwa wazungumzaji wazawa wa lahaja ya Kiimenti. Utafiti ulibainisha kuwa kuna michakato mingi ya kifonolojia inayopatikana katika vivumishi vya Kiimenti. Michakato hiyo huathiri irabu na konsonanti katika muundo wa vivumishi vya lahaja husika. makala hii itakuza na kuendeleza usomi wa vivumishi katika lugha mbalimbali za Kiafrika. Uelewa wa michakato ya kifonolojia inayoathiri irabu utasaidia kueleza kikamilifu muundo wa vivumishi vya Kiimenti na kuchochea utafiti zaidi kuhusu muundo wa vivumishi katika lugha za Kiafrika.

Downloads

Published

2023-05-31

How to Cite

Thuranira, K. K., Ontieri, J., & Ayodi, N. (2023). MICHAKATO YA KIFONOLOJIA INAYOATHIRI IRABU KATIKA MUUNDO WA VIVUMISHI VYA LUGHA ZA MNYAMBULIKO: MIFANO KUTOKA KIIMENTI. JARIDA LA MNYAMPALA, 3(1), 17–40. Retrieved from https://journals.sjut.ac.tz/index.php/mnyampala/article/view/19

Issue

Section

ARTICLES