MAUDHUI KATIKA NYIMBO ZA TOHARA ZA WAMASAABA NCHINI UGANDA
Abstract
Makala hii inaeleza maudhui mbalimbali yanayopatikana katika nyimbo za tohara za Wamasaaba nchini Uganda. Kulingana na wataalamu mbalimbali wa fasihi, maudhui ni mambo muhimu yanayopatikana katika kazi za sanaa. Nyimbo za tohara ni miongoni mwa kazi za sanaa ambazo hutekelezwa na binadamu. Katika makala hii, mwandishi anazingatia nadharia ya ethnografia na utendaji ambayo inalenga watu na ubunifu wao. Kwa kuzingatia nadharia hii, mwandishi anaeleza jinsi wanasanaa mbalimbali wanavyobuni nyimbo ili kuwasilisha mawazo yao. Mwandishi anafanya hivyo kwa kurejelea angalau mfano mmoja wa nyimbo hizo kwa kila maudhui. Mwandishi amepanga maudhui hayo kulingana na utaratibu wa utendaji wa nyimbo hizo za tohara. Kutokana na jambo hili, mwandishi anaangalia mambo mbalimbali katika utekelezaji wa tohara kwa sababu nyimbo hizo huambatana na matendo fulani. Hapa, mwandishi ametaja tendo linalotekelezwa na kutoa mfano wa wimbo unaoimbwa. Baada ya kutoa mfano wa wimbo, anauchanganua na kubainisha maudhui yaliyomo. Maudhui yanayowasilishwa yanaonesha mchakato mzima wa utendaji wa tohara kuanzia siku ya kwanza hadi ya tatu, wakati ambapo utendaji wa tohara yenyewe hukamilika. Nyimbo ambazo zimenukuliwa zinaonesha mambo kama vile: matayarisho ya tohara, vijana kuzuru ugenini, vijana kuondoka ugenini, vijana kujipa hamasa, na vijana kuondolea jamaa zao wasiwasi.