UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA MOFOLOJIA PAMOJA NA UMILISI WA KIWANGO CHA CHINI MIONGONI MWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU NCHINI UGANDA
Abstract
Ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya isimu katika lugha ya Kiswahili vyuoni umeathiriwa na changamoto kadhaa. Miongoni mwazo ni matumizi ya misamiati ya kisayansi ambayo imeathiri upataji na ukuaji wa umilisi wa taaluma za kiisimu. Makala hii inalenga kufafanua dhana muhimu katika uchunguzi na uchambuzi wa mofolojia, kuonesha changamoto za ujifunzaji na ufundishaji wake, na kutoa mapendekezo ya kuondokana na changamoto hizo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Uganda na kwingineko. Data ilikusanywa kupitia kwa mijadala shirikishi na usaili kutoka kwa wanafunzi 70 na walimu 9 wa isimu walioteuliwa kimaksudi kutoka katika vyuo vikuu vitatu nchini Uganda. Matokeo yaliyoelezwa kwa muundo wa kimaelezo yalidhihirisha changamoto za kiisimu na zisizo za kiisimu zilizoathiri upataji wa umilisi wa somo la mofolojia. Nazo ni pamoja na: umilisi wa chini katika matumizi ya Kiswahili sanifu, ugumu na kukanganywa katika kueleza dhana za kimofolojia, mitazamo hasi, pamoja na uchache wa vitabu vya isimu vinavyokidhi masilahi ya wanafunzi wa viwango vyote vya umilisi. Utafiti ulipendekeza kuwapo kwa mijadala na makongamano, uandishi wa vitabu mwafaka vya isimu, na kujenga uchanya wa ujifunzaji wa somo la mofolojia.