UFUTUHI: SILAHA YA JADI ILIYOTUMIWA NA SHAABAN ROBERT KUPAMBANA NA UKOLONI
Keywords:
Ufutuhi, Ujadi, UkoloniAbstract
Makala hii inabainisha namna mbinu ya ufutuhi ilivyotumika kama silaha ya kijadi ya kupambana na ukoloni. Utafiti uliozalisha makala hii ulitumia Nadharia ya Uhemenitiki. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu mbili, usaili na uchambuzi wa matini, kisha kuchanganuliwa kwa kutumia mbinu ya usimbishaji wa maudhui. Inabainishwa katika makala hii kuwa riwaya ya Kusadikika ni shambulizi kali lililoelekezwa kwa wakoloni, ambapo Shaaban Robert anabeua na kuing’ong’a mifumo ya kikoloni. Aidha, anaizindua jamii kuhusu umuhimu wa kujipapatua kutoka kwenye mikatale ya kikoloni. Kutokana na miktadha mbalimbali ya kikoloni iliyokuwa inamzunguka, aliweza kupenyeza shambulizi kwa maadui zake kwa kutumia aina nne za ufutuhi: ufutuhi wa majazi, ufutuhi wa balagha, ufutuhi wa unyume, na ufutuhi wa utanakuzi. Makala inahitimisha kwa kuwahamasisha waandishi ambao ni miongoni mwa makundi yanayotegemewa zaidi na jamii katika kuiongoza, kuikosoa, na kuiokomboa, kuendelea kuvaa ujasiri wa kufanya kazi yao kwa kutumia mbinu anuwai.