DAVID MASSAMBA: MWANAISIMU MWENYE HAZINA FICHE KATIKA FASIHI YA KISWAHILI
Keywords:
Mwanaisimu, Hazina Fiche, Utunzi wa Ushairi, DiwaniAbstract
Watu wengi wanamfahamu Hayati Prof. David Massamba kama mwanazuoni aliyemakinikia uga wa isimu kwa kiwango kikubwa huku baadhi ya vitabu vyake vikiwa maarufu katika ulimwengu wa Kiswahili. Hata hivyo, lipo jambo ambalo watu wengi hawalijui kwa mwanazuoni huyu; nalo ni suala la kujikita kwake katika kuandika kazi za kifasihi, hususani uga wa ushairi. Kwa hiyo, lengo la makala hii ni kubainisha na kuelezea hazina iliyojificha ya Massamba ili watu wapate kuijua na kuitumia kama ambavyo wanatumia maarifa yake ya isimu. Makala hii ni matokeo ya utafiti wa maktabani ambapo waandishi wametalii kazi mbalimbali za Massamba katika isimu na fasihi. Data zimechanganuliwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli chini ya Nadharia ya Uwasifu. Imebainika kwamba Massamba ana hazina fiche katika fasihi hususani katika ushairi wa Kiswahili ambapo ameandika Diwani ya Massamba na makala ya kinadharia inayohusiana na utunzi wa ushairi wa Kiswahili. Makala hii imejaribu kutoa muhtasari wa kazi hizo ili kuwahamasisha watu kusoma na kujipatia maarifa yaliyomo katika kazi hizo za kifasihi za Massamba.