UKALIMANI KATIKA MAHUBIRI KANISANI: UPOTOSHI AU UPANUZI WA MAANA?
Keywords:
Usemi Asilia (UA), Usemi Tafsiri (UT), Matini Chanzi (MC), Matini Lengwa (ML), Ukalimani, Tafsiri, FasiriAbstract
Makala hii inachunguza mchango wa dini katika lugha ya Kiswahili. Mchango wa dini katika maisha ya binadamu huwamba nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Dini imekuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya Kiswahili, hasa kupitia tafsiri na ukalimani, tangu enzi za ukoloni na ujio wa Wamishonari. Ukalimani wa kijamii, hususan katika mahubiri, huathiri Kiswahili ama kwa kukikuza au kukidumaza kimsamiati na kisarufi. Wakati mwingine, mkalimani hukosa muda wa kupitia na kusahihisha tafsiri yake, na kuleta tafsiri isiyokusudiwa. Mbali na umilisi wa lugha chanzi na pokezi, tafsiri humhitaji mfasiri kusomea tafsiri. Kwa hiyo, ukosefu wa muda hauwezi kuwa idhini kwa mkalimani kutepetea kwa sababu ujumbe unaokusudiwa na mzungumzaji ndio huwa muhimu zaidi. Mahubiri yanapokalimaniwa, lugha hutumiwa kiholela, na wakati mwingine inabadilisha maana inayokusudiwa. Lengo la makala hii ni kubainisha matumizi maalum ya lugha katika tafsiri za kidini, kutathmini iwapo matumizi hayo yanapanua au kupotosha Kiswahili kimsamiati na kimaana, na kutoa mapendekezo yatakayoboresha ukalimani wa mahubiri ya kidini ili kuchangia ukuaji wa lugha ya Kiswahili. Uchunguzi umejikita katika makanisa ya kiroho mjini Kakamega ambako mahubiri yalisikilizwa na kurekodiwa katika miktadha yake ya asili. Katika utafiti huu, data zilikusanywa kwa njia ya usikilizaji na kurekodi mahubiri katika miktadha yake ya asili. Kisha, muundo wa kimaelezo ulitumika kuchanganua data ili kutoa uelewa wa athari za ukalimani katika maendeleo ya Kiswahili.